HabariMilele FmSwahili

Rais Bouteflika wa Algeria asitisha azma yake ya kuwania urais baada ya maandamano nchini humo

Baada ya mashinikizo na maandamano ya karibu mwezi mmoja, hatimaye rais Abdelaziz Bouteflka wa Algeria amefutilia mbali azma yake ya kugombea tena urais katika uchaguzi ujao nchini humo. Bouteflika alitoa tangazo hilo jana jioni na kuongeza kuwa, uchaguzi huo uliotazamiwa kufanyika mwezi ujao wa Aprili utasogezwa mbele kidogo, kwa ajili ya kutoa fursa ya kufanyika kongamano la kitaifa kuhusu mustakabali wa kisiasa nchini humo.

Tangazo hilo la Bouteflika la kutogombea urais katika uchaguzi ujao nchini Algeria liliwaripua vijana ambao walimiminika barabarani usiku wa kuamkia leo kusherehekea kile walichokitaja kama ‘ushindi wa maandamano yao’. Kabla ya tangazo hilo, mamia ya mahakimu wa nchi hiyo walitoa taarifa na kueleza bayana kwamba, hawatosimamia uchaguzi wa rais wa Aprili 18 ikiwa Bouteflika ataamua kuwania tena kiti hicho kwa mara ya tano mfululizo, na kukaidi wito wa upinzani mkubwa wa wananchi wanaomtaka aachane na azma yake hiyo.

Show More

Related Articles