Mediamax Network Limited

Shilingi Bilioni 1.2 Kutumika Kuujenga Upya Uwanja Wa Mombasa.

 

Shilingi bilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili yakuujenga upya uwanja wa kaunti ya Mombasa ambao kufikia sasa uko katika hali yakutamausha.

Akitoa tamko hilo afisini mwake alipokutana na wajumbe wa tuzo za SOYA gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amewahakikishia wanamichezo kuwa uwanja huo wenye historia ndefu utajengwa upya ili kuufanya katika hadhi ya kimataifa.

Gavana Joho kadhalika amekinzana na wapinzani wake wanaozidi kumkashifu kuhusiana na kutokarabatiwa kwa uwanja huo akisema awamu yake ya kwanza kama gavana ilikua ngumu kidogo lakini sasa atahakikisha kila kitu kinakua sawa na anasema karibuni atatangaza nafasi za zabuni kwa wanakandarasi watakao shughulikia ujenzi wa uwanja huo.

Uwanja wa kaunti ya Mombasa umekua mahame kwa siku nyingi na kumekua na vilio kutoka kwa washikadau wamichezo lakini sasa nuru imeonekana na gavana Joho anasema uwanja huo utapanuliwa kuweza kukidhi mashabiki kati ya elfu kumi hadi kumi na tano.